Ufaransa kuvaana na Ujerumani

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ufaransa 2-0 Nigeria

Ufaransa imefuzu kwa mkondo wa robo fainali ya kombe la dunia baada ya kuilaza Super Eagles ya Nigeria mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa Brasilia.

Paul Pogba ndiye aliyeifungia Ufaransa bao la kwanza kunako dakika ya 79 ya mechi hiyo kupitia kichwa baada ya kipa wa Nigeria Vincent Enyeama kuutema mpira wa kona na kumtnuku Pogba na fursa ya kuwaweka vijana wa Didier Deschamps mbele.

Nigeria itajilaumu yenewe kwa bao hilo kutokana na makosa ya kimsingi ya safu ya ulinzi ambayo haikumakinika katika dakika za mwishomwisho ya mechi hiyo.

Maji yalizidi unga kwa Nigeria ,Dakika chache baadaye Joseph Yobo alipojifunga mwenyewe kufuatia shinikizo la wafaransa Griezmann baada ya Peter Odemwinge kugonga mpira nje na ukawa kona ambayo safu ya ulinzi ilishindwa kuhimili.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ufaransa sasa itachuana na Ujerumani katika robo fainali ya kombe la dunia

Kufuatia ushindi huo Ufaransa ilijikatia tikiti ya moja kwa moja hadi kwenye mkondo ujao wa robo fainali ya kombe la dunia ambapo sasa imeratibiwa kuchuana dhidi ya Ujerumani.

Vile vile kuondolewa kwa mabingwa hao wa Afrika sasa kumeiacha bara zima la Afrika bila ya mwakilishi katika mkondo ujao wa robo fainali baada ya Algeria kufurushwa na Ujerumani katika mechi nyengine 2-1.

Ujerumani ilipata mwaliko huo wa robo fainali baada ya kuibana mwakilishi mwengine wa Afrika Algeria ,mabao 2-1 katika mechi iliyoishia katika mmuda wa ziada .

Mechi hiyo ilikuwa imekamilika suluhu bin suluhu katika muda wa kawaida.