Brazil Kuonana na Colombia

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Neymar wa Brazil na Rodriguez wa Colombia

Timu mbili za kwanza zitakazoingia katika mkondo wa michuano ya nusu fainali zitajulikana baadaye leo. Ufaransa itachuana na Ujerumani huko Rio de Janeiro na wenyeji, Brazil kuchuana na Colombia huko Fortaleza.

Neymar wa Brazil dhidi ya James Rodriguez wa Colombia; hivi ndivyo mechi hii imeitwa, kwani wawili hawa ndio waliofunga mabao mengi kabisa hadi sasa katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2014 na pia wametajwa kuwa nyota wakubwa katika michuano hii.

Wawili hawa watakutana pale ambapo timu zao zitakapochuana kuwania nafasi katika timu nne za mwisho katika kombe la dunia.

Kibarua kigumu kiko kwa nchi inayoandaa michuano hii, Brazil, na Neymar mwenye umri wa miaka 22 ana mzigo mkubwa zaidi mabegani mwake.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mchezaji nyota wa Brazil Neymar na mashabiki

Baada ya kuishinda Chile kupitia mikwaju ya penalti, tukio lililokuwa la kuchosha na pia kuibua machozi, kwani wachezaji kadhaa wa Brazil walisalia na machozi, swali ambalo limeibuka ni, ni kiasi kipi ambacho wachezaji hawa wanaweza kuhimili.

Hata hivyo wanasisitiza wako tayari kuchuana na Colombia, ambao wamewafurahisha na kuwashangaza wengi, kwa mchezo wao.

Kwa hivyo mchuano huo mwingine wa siku, wahusisha timu mbili kutoka Marekani ya Kusini na mshindi bila shaka atapata nafasi kushiriki michuano ya nusu fainali dhidi ya moja kati ya timu za Ufaransa na Ujerumani, zinazochuana katika mechi ya kwanza huko Rio.