Suarez huenda akashiriki El Clasico.

Haki miliki ya picha FC Barcelona
Image caption Mshambulizi mpya wa Barca Suarez

Mshambulizi wa Uruguay na Barcelona huenda Luiz Suarez huenda akashiriki katika mechi dhidi ya Real Madrid mwezi Oktoba.

Suarez ambaye alitia sahihi kandarasi ya kujiunga na Barcelona punde baada ya kuondolewa katika kombe la dunia kwa tuhuma za kumng'ata mlinzi wa Italia Giorgio Chiellini alipigwa marufuku na FIFA kwa muda wa miezi minne.

Kandarasi hiyo iliigharimu Barca zaidi ya pauni milioni £75.

Suarez alipigwa marufuku tarehe 26 Juni siku mbili baada ya tukio kumaanisha kuwa atakuwa huru kurejea tarehe 26 Oktoba katika mkondo wa kwanza wa mechi ya El Clasico katika uwanja wa Bernabeu.

Mkondo wa pili utakuwa tarehe 22 machi mwakani.

Hata hivyo Mshambulizi huyo zamani akiichezea Liverpool hataweza kufanya mazoezi na timu hiyo kwani angali anatumikia marufuku ambayo inamzuia kushiriki mechi yeyote ile wala kuingia katika uwanja wowote ule wa kandanda.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Suarez alipomng'ata Chiellini katika kombe la dunia Brazil

Kulingana na Ratiba ya mechi za La Liga , mabingwa watetezi wa ligi hiyo Atletico Madrid watafungua kampeini ya kutetea taji lao dhidi ya Rayo Vallecano Agosti tarehe 24 ,Huku Barca ikifungua kampeini ya mwaka huu kwa kuialika Elche nyumbani kwao .

Mabingwa wa Ulaya Real Madrid nao watakuwa wenyeji wa Cordoba katika mechi yao ya ufunguzi.

Je Real itampa mfungaji mabao mengi katika kombe la dunia mwaka huu James Rodriguez nafasi katika el Clasico ?

Ama mabingwa hao watamchezesha mjerumani Toni Kroos?

Wasimamizi wa ligi hiyo ya Uhispania wanatarajiwa kuamua wiki hii iwapo watatumia povu nyeupe kama iliyotumika katika kombe la dunia kuhakikisha mahala mpira unapaswa kuwekwa ama wapi laini ya walinzi inapaswa kupigwa wakati wa free-kick .