Mnaigeria agundulika kutumia dawa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Chika Amalaha

Mshindi wa medali ya dhahabu toka Nigeria Chika Amalaha amesimamishwa kwa muda kushiriki kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola baada ya vipimo kuonyesha kuwa alitumia dawa za kuongeza nguvu.

Binti huyo mwenye umri wa miaka 16,alishinda medali ya dhahabu katika kunyanyua vitu vizito baada ya kuinua uzito wa jumla ya kilo 196,kwa upande wa wanawake wenye uzito wa kilo 53.

Vipimo vya awali alivyofanyiwa vilionyesha kuwa ametumia dawa aina ya Amilorde na hydrochlorothiazide ,ambazo zote zimepigwa arufuku michezoni.

Binti huyo anatarajiwa kuchukuliwa kipimo cha pili hapo kesho jumatano.

Mwanariadha huyo chipukizi wa Nigeria alishinda medali ya dhahabu Ijumaa iliyopita huku Dika Toua akiipatia Papua New Guinea medali ya ya kwanza kwenye michezo hii ya Jumuiya ya madola mwaka huu inayoendelea mjini Glasgow,ambapo Santoshi Matsa wa India aliipatia medali ya Shaba nchi yake kwea kushika nafasi ya tatu.

Amalala ni mwanariadha wa kwanza kugundulika kutumia dawa za kuongeza nguvu kwenye michezo hiyo ya jumuiya madola,ambapo Mwanariadha wa mbio za kuruka viunzi mita 400 Rhys Williams kutoka Wales,na mkimbiaji wa mbio za Mita 800 Gareth Warburton pia wa Wales wakiwa wamelazimika kukosa michuano hiyo kutokana na kukabiliwa na tuhuma za matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Wanariadha wote hao wanakanusha kutumia dawa yoyote iliyopigwa marufuku huku wakiwa wanafahamu.