Man U yaanza ligi kwa kichapo

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wachezajii wa Manchester United wakitoka kwa huzuni baada ya kukubali kichapo cha 2-1 kutoka Swansea

Manchester United imeanza vibaya katika msimu huu wa ligi kuu ya England baada ya kukubali kichapo cha magoli 2 - 1 dhidi ya Swansea.

Swansea ndio waliokuwa kwanza kuandika bao katika dakika ya 28 kipindi cha kwanza bao lilofungwa na Ki Sung Yueng.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika Manchester United walikuwa nyuma kwa bao 1 - 0.

Baada ya kutoka mapunziko Man U walionekana kuja kwa kasi ambapo walilishambulia lango la Swansea mara mara na ndipo katika dakika ya 53 Nahodha mpya wa timu hiyo Wayne Rooney akafanikiwa kusawazisha goli kwa kuunganisha mpira wa kona.

Hata hivyo kama vile waswahili wasemavyo siku ya kufa nyani miti yote huteleza, dakika ya 72 Gyfi Sigurdsson wa Swansea baada ya walinzi wa Manchester United kujichanganya alipigilia msumari wa moto kwenye kidonda na kuandika bao la ushindi kwa Swansea na hivyo kufanya hadi mechi inamalizika Manchester United ikawa imefungwa 2 - 1.

.