Libya yajiondoa kuandaa AFCON2017

Haki miliki ya picha epa
Image caption Libya imekiri usalama umedorora

Libya imejiondoa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kuwania kuwa mabingwa wa Afrika mwaka wa 2017.

Ujumbe wa taifa hilo lililogubikwa na vita limesema kuwa vita vinavyoendelea nchini humo vimewanyima fursa ya kujenga viwanja na makao ya timu zitakazoshiriki mashindano hayo.

Kufuatia kauli hiyo shirikisho la soka barani Afrika CAF sasa limeomba mataifa badala kutuma maombi ya kutaka kuwa wenyeji wa mashindano hayo yanayohusisha timu 16.

Mataifa yanayotaka kuandaa mashindano hayo yana muda wa hadi septemba tarehe 30 kutuma maombi yao.

Caf itatangaza mwenyeji mpya wa mashindano hayo mwakani.

Shirikisho la CAF linasema kuwa linatafuta taifa lenye uwezo wa kuhakikishia washiriki makao usalama viwanja na muundo msingi bora wa usafiri wao .

Image caption Mapigano baina ya makundi tofauti yamesababisha mashindano kuahirishwa.

Serikali ya Libya inakabiliwa na changamoto ya usalama baada ya makundi ya wapiganaji yaliyopewa silaha ilikumng'oa aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo kwa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka wa 2011 kukataa kusalimisha silaha zao.

Libya ilikuwa imeahidi kujenga viwanja 11 kwa gharama ya dola milioni 314 za Marekani ikiwemo uwanja wenye viti 60,000 uliokuwa unastahili kujengwa katika kambi ya zamani ya jeshi mjini Tripoli.

Miji ya Benghazi na Misrata ilikuwa imeratibiwa kujengewa viwanja vipya lakini miji hiyo ndiyo iliyokuwa chimbuko la vita vilivyomng'oa mamalakani Gaddafi.

Tayari ligi kuu ya Libya imeahirishwa kwa hofu ya kuwa timu shiriki zitashindwa kuhakikishia usalama wao.

Image caption Mataifa yenye uwezo wa kuandaa makala ya 2017 ya AFCON yana mwezi mmoja kutuma maombi yao

Mechi zote za kimataifa zinahusisha libya kwa sasa zinaandaliwa katika taifa jirani la Tunisia.

Sadfa ni kuwa kwa mara ya kwanza Libya ndiyo iliyotawazwa mabingwa wa kombe la Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani yaani CHAN .

Vilevile Caf inatarajiwa kutangaza mwenyeji wa makala ya mwaka wa 2019 na 2021 katika mkutano wake mkuu utakaoandaliwa mjini Addis Ababa Ethiopia 20 Septemba.

Algeria, Cameroon, Guinea, Ivory Coast na Zambia zimetangaza azimio la kuandaa mashindano hayo.