Michuano ya magongo Kenya

Image caption Mshindi wa mashindano haya ya kufuzu atacheza katika fainali Rio De Janeiro mwaka 2016

Mashindano ya mchezo wa magongo ya ligi ya dunia yanaanza Ijumaa wiki hii mjini Nairobi katika uwanja wa City Park.

Mataifa yanayowakilishwa ni wenyeji Kenya, Misri, Ghana na Tanzania. Nigeria ilijiondoa kutokana na ugonjwa wa Ebola uliotikisa kanda ya Afrika Magharibi.

Mechi ya kwanza Ijumaa ya wanawake ni kati ya Ghana na Tanzania ikifuatiwa na mbili za wanaume kati ya Misri na Ghana kisha Kenya dhidi ya Tanzania.

Siku ya pili Jumamosi timu ya wanawake ya Kenya inacheza na Ghana na baadae mechi mbili za wanaume, ya kwanza Misri dhidi ya Tanzania na Ghana inakutana na Kenya.

Jumapili mechi ya kwanza ya wanawake ni kati ya Tanzania na Kenya..kwa upande wa wanaume ni Ghana dhidi ya Tanzania na Kenya ikitoana jasho na Misri kwenye mechi inayotarajiwa iwe ya kukata na shoka.

Kulingana na mwenyekiti wa chama cha mchezo wa magongo cha Kenya Nashon Randiek mshindi wa mashindano ya Nairobi atafuzu kushiriki mengine kama hayo lakini na timu za hadhi ya juu nchini Afrika Kusini mwakani mwezi machi.

Washindi nchini Afrika Kusini watasonga mbele na hatimaye mataifa yatakayoshinda yatafuzu kwa michezo ya Olympiki mwaka wa 2016 mjini Rio De Janeiro.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa chama cha kriketi cha kenya Jackie Janmohammed amejerea tena uongozini baada ya kujiuzulu mwezi julai kwa sababu za kibafsi.

Jackie ni mwanamke wa kwanza duniani kuongoza chama cha kriketi cha taifa.