Bale aipa ushindi Wales

Haki miliki ya picha real madrid on twitter
Image caption Gareth Bale

Mshambuliaji Gareth Bale ameifungia timu yake ya taifa ya Wales mabao 2 dhidi ya Andora.

Katika mchezo huo wa kusaka tiketi za fainali kombe la Mataifa ya Ulaya, Iliwagharimu Andora dakika 6 tu kujipatia bao lao la kwanza kabisa katika mchezo wa mashindano tangu mwaka 2010.

Hata hivyo mshambuliaji huyo nyota wa Real Madrid alifanya kile kilichosubiriwa na mashabiki wa nchi yake alipoisawazishia Wales na kufunga bao lingine la pili katika dakika za lala salama na kutoka kifua mbele kwa pointi tatu.

Kwenye mechi zingine kumekuwa na matokeo ya kushangaza, ambapo Iceland wameiadhibu vikali Uturuki kwa mabao 3-0, huku kocha wa Uholanzi Guus Hiddink akiteswa na kichapo cha pili mfululizo tangu achukue timu hiyo kutoka kwa Louice Van Gal.

Uholanzi ikicheza ugenini mjini Prague imepigwa mwereka na Jamhuri ya Czech kwa mabao 2-1.

Mabao ya Simone Zaza na Leonardo Bonucci yameipatia Azzurri timu ya Taifa ya Italia ushindi wa mabao 2-0 wakiwa ugenini kwa kuichapa Norway. Nao Croatia wakiwaning'iniza Malta waliomazia mchezo wakiwa pungufu kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Luka Modric na Andrei Kramaric..huku Cyprus ikijitoa mkosi kwa kuichapa 2-1 Bosnia Herzogovina.