Cameroon kuwa mwenyeji wa S.Leone

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Cameroon imekubali ombi la Sierra Leone kuwa mwenyeji wa mechi ya AFCON2015

Cameroon imekubali ombi la Sierra Leone la kuandaa mechi ya kufuzu kwa kombe la Afrika mwakani .

Sierra Leone imeruhusiwa kuandaa mechi yake ya nyumbani katika mji wa Yaounde tarehe 10 Oktoba.

Awali mechi hiyo iliratibiwa kuchezwa nchini Sierra Leone lakini Shirikisho la kandanda la Afrika (CAF) likatangaza marufuku ya mechi zozote kufanyika nchini humo kutokana na tishio la mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Kauli hiyo inamaanisha Cameroon itaialika Sierra Leone mara mbili mjini Yaounde katika muda wa siku nne.

The Indomitable lions watakuwa wenyeji wa Leone Stars katika mechi ya marudiano ya kundi D tarehe 15 Oktoba.

Katibu mkuu wa shirikisho la kadanda la Cameroon Tombi a Roko Sidiki, amesema , baada ya kushauriana na waziri wa Michezo, shirikisho hilo limekubali kuandaa mechi zote mbili mjini Yaounde kwa minajili ya kuonyesha umoja na Taifa hilo lililoathirika pakubwa na ugonjwa wa Ebola.

Mwezi uliopita, mechi iliyoratibiwa kuchezewa nchini Sierra Leone iliahirishwa na kuilazimu Leone Star kusafiri mpaka nchini Congo kucheza dhidi ya timu ya taifa ya DRC mjini Lubumbashi.

Leone Star ilifungwa 2-0.

Hapo awali walikuwa wamelazwa na timu ya Ivory Coast mabao 2-1.

Matokeo hayo yasiyo ya kupendeza yameiacha timu ya Leone star ikishika mkia wa kundi D na kumfanya aliyekuwa mkufunzi wao Johnny McKinstry kupoteza kazi yake kama kocha.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ebola imeathiri pakubwa hali ya kawaida ya maisha ya raiya wa Sierra Leone

Atto Mensah ndiye aliyechukua wadhfa wa kuiongoza timu hiyo juma lililopita.

Kulingana na orodha ya Fifa ya timu bora , inaonyesha timu ya Leone star imeshuka kutoka nafasi ya 50 mpaka 70.