Taathimini ya ligi kuu ya EPL

Haki miliki ya picha PA
Image caption Ndoto ya van Gaal kutamba ilitibuka

Matumaini ya mkufunzi wa Manchester United Van Gaal kuendelea kufanya vyema baada ya kuilaza QPR mabao 4-0 juma lililopita yalikatizwa

ghafla hapo jumamosi Manchester United iliponyukwa mabao 5-3 na timu changa ya Leicester City.

Timu hiyo yenye vijana machachari ilionyesha mchezo wa hali ya juu na hivyo kutia kibindoni alama tatu muhimu.

Timu ya Manchester United ilibaki kinywa wazi kutokana na kichapo hicho huku Leonardo Ulloa na Esteban Cambiasso raia wa Argentina wakifunga mabao matatu kati ya mabao matano yaliyofungwa.

Mkufunzi wa Manchester United Vaan Gal aliilaumu timu yake kwa kusema walicheza ovyo.

Liverpool hali halisi

Baada ya kushindwa mara ya tatu na timu ya West Ham 3-1 katika mechi zake tano za kwanza, mkufunzi wa Liverpool Brendan Rodgers

ameiomba timu yake kuelewa matarajio ya washikadau ni makubwa kwani inashiriki katika ligi ya mabingwa ulaya.

‘‘Timu zote zimekuwa zikitamani kutushinda lakini tumeonyesha upinzani mkali.

Lazimu tuelewe hali hii”, Rodgers alisema.

Timu ya Liverpool ilirudi katika ligi ya Mabingwa Ulaya jumanne iliyopita kwa kishindo na kuigaragaza timu ya Ludogrets Razgrad mabao 2-1.

Hata hivyo, Rodgers amekiri kwamba timu hiyo imeanza msimu kwa hali ngumu na hivyo inabidi watie bidii.

Penzi la Lampard kwa Chelsea laisha

Kiungo,Frank Lampard anayeichezea timu ya Manchester City kwa mkopo kutoka klabu ya Marekani aliisawazishia timu yake baada ya kufunga bao moja dhidi ya timu yake ya zamani Chelsea katika mechi ya kukata na shoka ya ligi ya EPL.

Bao hilo liliinyima Chelsea nafasi ya kupata alama tatu muhimu ambazo zingeifanya kupanda ngazi kwa alama tano.

Kulingana na mkufunzi wa Chelsea Jose Mourinho hili lilionyesha wazi kwamba penzi la Lampard kwa Chelsea halipo tena.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Dakika nne za mashambulizi makali za mfurahisha Wenger

Dakika nne za mashambulizi makali zamfurahisha Wenger

Timu ya Arsenal ambayo imetoka sare katika mechi zake tatu katika ligi ya Uingereza ilionyesha makali yake hapo jumani baada ya kuitandika timu ya Aston Villa mabao 3-0.

Mabao hayo yalifungwa kwa ufundi mkubwa katika muda wa dakika nne pekee.

Bao la kwanza lilitiwa kinywani na mchezaji matata kutoka Ujerumani Mesut Ozil huku mchezaji mpya wa Arsenal Danny Wellbeck akifunga ukurasa kwa bao lake lililoipa arsenal ushindi.

Mkufunzi wa Arsenal, Arsene Wenger amesema alifurahishwa sana na timu yake na kuongeza kwamba sasa ipo tayari kufanya vyema zaidi.

Wachezaji kutoka Afrika washamiri

Image caption Wanyama alifunga bao lake la kwanza la Southampton

Wachezaji nyota kutoka afrika walizidi kutamba katika ligi ya Uingereza kwa kuzifungia timu zao mabao.

Katika mechi kati ya Newcastle and Hull city iliyoisha sare ya 2-2, mchezaji kutoka Senegal Papiss Cisse aliifungia Newcastle mabao yote mawili huku raia mwenzake wa Senegal Mohamed Diame akiifungia Hull city bao moja.

Diafra Sakho kutoka Senegal liifungia timu yake West Ham bao dhidi ya Liverpool na kuiwezesha kushinda mechi hiyo mabao 3-1.

Kiungo wa kati, ambaye ni raia wa Kenya, Victor Wanyama anayeichezea timu ya Southampton alifunga bao lake la kwanza na kuiwezesha timu yake kuinyuka Swansea bao 1-0.

Wakati huo huo mchezaji wa Crystal Palace ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Yannick Bolasie aliipatia timu yake ushindi wa kwanza msimu huu dhidi ya Everton.