Uingereza kufanya uamuzi kuhusu ISIS

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wabunge wakimsikiza waziri mkuu David Cameron

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amewasilisha mswada bungeni wa kuiruhusu UK kuungana na Marekani katika mashambulizi ya angani dhidi ya wapiganaji wa Islamic State.

Chama cha Tories, Liberal Democrats na Labour vinaunga mkono hatua hiyo vikisema inakubalika kisheria kwa kuwa serikali ya Iraq ndiyo iliyoomba usaidizi wao.

Wapiganaji wa IS wameweza kudhibiti maeneo mengi nchini Iraq na Syria katika miezi ya hivi karibuni.

Kundi hilo linaloitwa pia Isis linatumia mbinu nyingi mojawapo ikiwa ile ya kuwakata vichwa wanajeshi, wanahabari kutoka marekani na pia wafanyakazi ya kutoa msaada.

Kwa mujibu wa Shirika la kijasusi la marekani CIA, wapiganaji hao huenda wamefikia 31,000.

Bunge hilo liliombwa kurudisha vikao vyake ili kujadili hatua za majeshi nchini Iraq, linatarajiwa kupiga kura hapo saa 17.30 BST ili kuamua kama Uingereza itashiriki vita hivyo.

Hii ni baada ya mjadala utakaochukua masaa saba.

Aidha,UK haipendekezi kushiriki katika mashambulizi ya angani dhidi ya Syria.

Hapo alhamisi angalau watu 250 waliandamana nje ya lango la Downing Street kupinga uwezekano wa kutumwa kwa wanajeshi nchini Iraq.

Baadhi ya wabunge pia wanapinga hatua hiyo.

Image caption Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron anawasihi wabunge kumruhusu kushambulia ISIS

Diane Abbott, Jeremy Corbyn na John McDonnell wa chama cha Labour wametia saini katika barua inayopelekwa kwa The Guardian inayosema Uingereza kushiriki katika kuishambulia Iraq kwa mabomu hakutafanya hali kuwa nzuri ila kutasababisha matatizo zaidi.

Serikali ya Uingereza haihitaji idhini wala ruhusa kutoka kwa wabunge ili kuanza mashambulizi ya kijeshi lakini umekuwa mtindo kuwasilisha mswada bungeni kwanza tangu kulipokuwa na vita nchini Iraq mwaka wa 2003.

Serikali ya Uingereza imesema ombi hilo la Iraq linatoa msingi wa kisheria kwa Uingereza kuanza mashambulizi ya angani.

Waziri mkuu wa Australia Tony Abbott amesema serikali yake itaamua siku zijazo kama itaungana na Marekani katika mashambulizi ya angani dhidi ya wapiganaji wa Islamic State nchini Iraq na Syria.