Hamu ya kocha wa vijana Guinea

Kocha wa kikosi cha timu ya Guinea ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17 anaamini kuwa timu hiyo ina uwezo wa kufuzu kwa kombe la dunia la vijana hao wenye umri huo mwaka ujao.

Vijana wa Camara, wenyewe wanaamini kuwa wana fursa nzuri ya kushiriki kombe la dunia la vijana hasa baada ya kuicharaza Togo mwishoni mwa wiki na kufuzu kwa mashindano ya kombe la taifa bingwa Afrika nchini Niger mwaka ujao.

Mashindano hayo ni moja ya njia za kuonyesha kipaji chao kwa dunia nzima huku timu nne zilizofuzu nusu fainali zikijiandaa kwenda kwa mchuano huo nchini Chile.

Guinea ilifanikiwa kufuzu baada ya kuicharaza Togo kwa bao moja bila, na kumaliza kibarua chao kwa kushinda mechi yao ya ugenini kwa mabao 3-0

Wataungana kwenye fainali na timu nyingine zilizofika fainali, kama Nigeria, Ghana, Ivory Coast, Zambia, Mali na Afrika Kusini washindi wengine wa awamu ya mwisho ya kufuzu pamoja na wenyeji Niger.

Baada ya ushindi wa Guinea, Camara aliambia BBC michezo kwamba:"Timu yoyote inayoshinda lazima isonge mbele kama tulivyofanya. Tuna hamu sana ya kushiriki michuano ya kombe la dunia. Hilo ndilo sisi tunalitamani sana. Tunataka mengi na ikiwa Mungu atatukubalia, tutafikia malengo yetu. ''

Camara pia alitupatia hakikisho lake kuwa timu yake itasaidiwa kifedha na serikali na haoni kama kutakuwa na tatizo lolote la kifedha.

Na alitabiri mafanikio kwa wachezaji wake kikanda na kimataifa.

"utajionea mwenyewe timu hii ya kitaifa, itaweza kufika fainali, '' alisema Camara.