FIFA yamuunga rais mpya wa soka Nigeria

Haki miliki ya picha AP
Image caption Sepp Blatter

Rais wa FIFA Sepp Blatter amemuunga mkono Amaju Pinnick kama rais mpya wa shirikisho la soka nchini Nigeria NFF.

Pinnick mwenye umri wa miaka 43 ambaye ni mwenyekiti wa tume ya michezo ya Delta Sport alichaguliwa siku ya jumanne.

Blatter amesema katika barua aliomuandikia Pinnick kwamba anamtakia mafanikio katika kazi yake mpya na kwamba anatarijia kukutana naye hivi karibuni.

Matamshi yake yameondoa hofu kwamba huenda taifa hilo likapigwa marufuku baada ya FIFA kutoidhinisha uchaguzi huo.

Shirikisho la soka duniani FIFA liliipatia marufuku ya mda Nigeria mnamo mwezi Julai baada ya aliyekuwa rais wa shirikisho la Nigeria Aminu Maigari kutimuliwa afisini,swala lililosababisha mgawanyiko huku Chris Giwa akijitangaza kama rais mpya,swala lililoishinikiza FIFA kutishia kuiwekea marufuku hiyo iwapo uchaguzi huo usingefanyika.

Kumekuwa na ripoti kwamba uchaguzi huo wa siku ya jumanne ulifanyika licha ya agizo la mahakama lililotolewa dhidi ya kundi linaloongozwa na Giwa.

Na baada ya uchaguzi huo Giwa alitoa taarifa akisisitiza kwamba bado ndiye kiongozi wa shirikisho hilo la Nigeria.