Andy Schleck ajiuzulu Tour de France

Haki miliki ya picha BBc
Image caption Waendesha baiskeli wa mashindano ya Tour de France

Bingwa wa zamani wa wa mbio za baiskeli za Tour de France Andy Schleck amestaafu katika mchezo huo akiwa na umri wa miaka 29 kwa sababu ya maumivu ya goti.

Mwendesha baiskeli huyo wa timu ya Trek Factory Racing hajaweza kupona maumivu ya goti aliloumia mjini London katika mzunguko wa tatu wa mashindano ya Tour de France 2014.

"Ningependa kuendelea kushindana lakini goti langu haliniruhusu," amesema.

Schleck alishinda taji la mwaka 2010 la Tour de France, ambapo mwaka 2012 Albert Contador kutoka Hispania alinyang'anywa taji hilo mwaka 2012 baada ya kugundulika kutumia dawa za kusisimua misuli ambazo zimepigwa marufuku kutumika michezoni.

Mchezaji huyo kutoka Luxembourg alimaliza katika nafasi ya pili katika mashindano ya Tour De France ya mwaka 2009 na 2011.

Schleck, ambaye aliumia karibu na viwanja vya Olympic Park mjini London katika siku ya mwisho ya mbio za siku tatu za Tour de France nchini Uingereza mwaka huu, amesema: "Tangu kuumia kwangu nchini Uingereza hakuna dalili ya kupata nafuu".

"Wakati misuli ikiwa imepona, gegedu ndio tatizo. Nimekuwa nikifanya bidii kutibu goti lakini nilikuja kutambua kuwa niko katika hatari ya kushindwa kupona iwapo nitaendelea na mbio hizi, huo ni uamuzi mzuri kabisa niliochukua wa kujiuzulu mchezo huu."