Kocha aliyefutwa kazi akataa kung'atuka

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Timu ya soka ya Sierra Leone

Atto Mensah amesisitiza kuwa yeye ndiye mkufunzi wa timu ya soka ya Sierra Leone licha ya ripoti kwamba John Sesay Ajina ameteuliwa kuwa kocha mpya wa kikosi hicho.

Sesay aliajiriwa ili kusimamia kikosi hicho dhidi ya Cameroon katika mechi ya kufuzu kwa kombe la taifa bora barani afrika.

Shrikisho la soka nchini Sierra Leone linaamini kuwa Mensah hajafuzu kusimamia michuano hiyo ya tarehe 11 na 15 mwezi Octoba.

lakini Mensah ameiambia BBC kwamba anaamini amefuzu kusimamia kikosi hicho na kwamba ametoa stakhabadhi zake zote kwa shirikisho hilo kuonyesha masomo ya ukufunzi aliyofanya. . Anasema kuwa amefanya mazoezi na kikosi hicho na yuko tayari kukiongoza.

Mensah aliteuliwa na shirikisho la soka nchini Sierra Leone pamoja na wizara ya michezo mnamo mwezi Septemba baada ya Johnny Mc Kinstry kufutwa kazi.

Lakini Shirikisho hilo linasema kuwa limemfuta kazi na nafasi yake kuchukuliwa na Sesay kama kaimu kocha ,huku Abdulai Bah akiwa naibu wake na kwamba wawili hao wanatarajiwa kuwasili mjini Younde siku ya alhamisi ili kuanza kuiongoza timu hiyo.