Mashabiki jela kwa kumkejeli Putin

Mahakama nchini Belarus, imewahukumu kifungo cha jela mashabiki wa soka kwa kuimba nyimbo za kumkejeli na kumtusi Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mwanamume mmoja alifungwa jela siku kumi kwa kuvalia nembo za kibaguzi. Wengine saba walifungwa jela kwa siku tano kwa kutumia lugha chafu.

Walikuwa wameungana na kuanza kuimba nyimbo za kumdharau Rais Putin katika mechi ya kufuzu kwa kombe la Euro mwaka 2016 kati ya Ukraine na Belarus.

Mashabiki kadhaa wa Bealrus pia walifungwa au kutozwa faini.

Mashabiki wote wa Belarus na Ukraine waliungana na kuimba wimbo ambao unasifika sana na ambao unaonyesha upinzani dhidi ya Rais Putin

Mashabiki wa Belarus pia walisikika wakisaidiana na wale wa Ukraine katika kumkejeli Putin.

Baada ya mechi hiyo mashabiki 100 wa Ukraine na 30 wa Belarus walikamatwa na kuzuiliwa kulingana na taarifa kwenye mtandao wa upinzani Charter '97.

Baadaye mahakama iliwafunga jela mashabiki hao wa Ukraine kwa siku tano kwa kutumia lugha chafu. Wengine wanne walitozwa faini wakati shabiki wa Ukraine akifungwa jela kwa siku kumi kwa madai ya kuvalia nembo ya baguzi ya swastika kwenye mavazi yake.

Sio mara ya kwanza kwa mashabiki kuimba nyimbo za kumkejeli Putin.

Mnamo mwezi Juni maafisa wa Urusi walitoa wito wa kustaafu kwa waziri wa maswala ya kigeni wa Ukraine Andriy Deshchytsya, baada ya kujiunga na maandamano mjini Kiev dhidi ya Putin.