Rais Jonathan ang'aka ye si mkwasi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria

Rais Goodluck Jonathan hivi karibuni ameng'aka kuwa jina lake kujumuishwa katika orodha ya marais tajiri Afrika haina msingi wowote na ina msingizia.

Pamoja na hayo rais Goodluck ametaka asafishwe kwenye vyombo vya habari na pia aombwe radhi katika website ambayo ilichapisha taarifa hiyo.

Website hiyo ilimuweka raisi huyo wa Nigeria katika nafasi ya sita kwa utajiri Africa unaokisiwa kuwa kiasi cha dola za kimarekani milioni miamoja.

Orodha hiyo yenye kuainisha maraisi tajiri wa mwaka 2014 imemuweka katika nafasi sawa Mfalme Mswati wa tatu wa Swaziland.

Wengine wanaoingia katika orodha hiyo kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tisa ,ni Jose Eduardo dos Santos wa Angola, King Mohammed wa sita wa Morocco, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea, Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya, Paul Biya wa Cameroun, Idriss Deby wa Chad, na Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Katika taarifa ya Rais Jonathan kupitia kwa msemaji wake, Dokta Reuben Abati, amesema kuwa kujumuishwa kwa jina la raisi kwenye orodha hiyo kunamtumbukiza moja kwa moja katika tuhuma za ulaji rushwa .

Kwa muujibu wa Abati, anadai kuwa hakuna vigezo vya kumuweka raisi Jonathan katika nafasi ya sita mkuu wa nchi ,huku ikifahamika wazi kuwa raisi huyo hajawahi kufanya biashara ya aina yoyote wakati katika umri wake ameishi kwa kuitumikia jamii yake kama mtumishi wa umma,na amekua katika ofisi za umma tangu mwaka 1999, na amekuwa akieleza wazi mali alizonazo kama ambavyo sheria za Nigeria zinavyotaka.

Website hiyo imeshinda kuonesha namna raisi Jonathan aliyetawala kwa miaka minne ni tajiri zaidi ya Deby na Mugabe ambao kwa pamoja wametawala kwa miaka 23 na 26 madarakani.