CAF:Hatujabadili tarehe ya michuano

Haki miliki ya picha CAF
Image caption CAF

Waandilizi wa dimba la taifa bora barani Afrika ACN wanasema kuwa hakuna mabadiliko yoyote ya tarehe ya michuano hiyo licha ya ombi la mwenyeji wa mechi hizo Morocco la kutaka michuano hiyo kuahirishwa.

Serikali ya Morrocco imeliandikia shirikisho la soka barani Afrika CAF ikilitaka kuahirisha mechi hizo kutoka january 17 hadi February 8 kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

CAF imesema kuwa italijadili ombi hilo katika mkutano ujao wa kamati kuu ya shirikisho hilo mnamo Novemba 2.

Baadaye rais wake Issa Hayatou atakutana na maafisa wa Morocco siku itakayofuata.

Zaidi ya watu 4000 wamepoteza maisha yao kutokana na ugonjwa wa Ebola ambao ulizuka katika eneo la Afrika Magharibi mwanzoni mwa mwaka huu.

Wizara ya afya nchini Morocco ilitoa ombi hilo siku ya ijumaa ili kuzuia matukio ambayo yanahusisha mataifa yalioathirika na ugonjwa wa ebola.

Siku ya jumamosi CAF ilijibu ombi hilo na kusema kuwa '' Caf imesajili ombi hilo na inasisitiza kuwa hakuna mabadiliko yoyote yaliofanyika kuhusu mashindano hayo'',.