Tanzania yaikomoa Benin 4-1

Image caption Timu ya Tanzania," Taifa Stars"

Timu ya Taifa ya Tanzania, "Taifa Stars" imeibuka na ushindi mnono dhidi ya Benin baada ya kuicharaza magoli 4-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa ulio katika kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani, FIFA.

Kabla ya mchezo uliopigwa katika dimba la uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam, Tanzania, Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya 115 katika viwango vya ubora vya Fifa duniani, ikishika nafasi ya 34 barani Afrika, huku Benin ikiwa katika nafasi ya 78 duniani na 18 barani Afrika.

Mabao ya Tanzania yalifungwa na Nadir Haroub Cannavaro, Amri Kiemba, Thomas Ulimwengu na Juma Luizio akiifungia timu yake magoli mawili, huku la kufutia machozi la Benin likitumbukizwa wavuni dakika ya 90 ya mchezo na Ssegnon Stephane anayechezea timu ya West Bromwich Albion ya England.

Katika uwanja huo huo wa Taifa kabla ya mchezo wa Tanzania na Benin, mchezo mwingine wa kuvutia ulizikutanisha timu za viongozi wa dini waliochanganyika katika timu mbili wakiwemo Mashekhe na Maaskofu.

Viongozi hao waliunda timu za Amani na Mshikamano, ambapo Amani waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mchezo huo ulilenga kuonyesha ushirikiano wa kijamii kati ya waumini wa dini kubwa mbili nchini Tanzania za Waislam na Wakristo.