Chris Katongo nje ya Chipolopolo

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Nahodha wa Chipolopolo Chris Katongo

Nahodha wa timu ya taifa ya kandanda ya Zambia, Chris Katongo ameondolewa katika kikosi cha Chipolopolo ambacho kimeratibiwa kuchuana na Timu ya taifa ya Niger katika michuano ya kufuzu kwa kombe la afrika hapo Jumatano.

Hii ni baada ya mchezaji huyo kutofautiana na wakufunzi.

Kiungo wa kati huyo aliiambia BBC kwamba amejiondoa katika kikosi hicho kinachofanya mazoezi mjini Ndola lakini akaakataa kutoa maelezo zaidi.

Mnamo Jumamosi katika mechi iliyotoka sare tasa kati ya zambia na Niger, Katongo aliingia uwanjani katika dakika ya 76 kama mchezaji wa akiba.

Matokeo hayo yaliiacha Zambia na pointi mbili sawa na Niger katika kundi F na hivyo kuwa nyuma ya Msumbiji na pointi tano na pia nyuma ya Viongozi wa kundi hilo Cape Verde kwa pointi sita.

Katongo ambaye aliwahi kushinda taji la mchezaji bora zaidi afrika katika shindano lililoandaliwa na BBC, alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Zambia mwaka 2012 wakati Zambia iliposhinda kombe la Afrika lililoandaliwa nchini Gabon na Equatorial Guinea.

Kwa sasa Katongo anaichezea timu moja ya Afrika kusini kadanda ya kulipwa baada ya kukigura klabu cha Henan Construction cha Uchina mwaka uliopita.