Kenya kushiriki kombe la walemavu

Image caption Kikosi cha Kenya kikiwa mazoezini

Kenya na Ghana ndiyo mataifa pekee kutoka Afrika yatakayoshiriki kwenye mashindano ya kombe la dunia ya kandanda ya walemavu nchini Mexico mwezi ujao.

Uzbekistan ndio bingwa mtetezi wa mashindano hayo yatakayojumuisha timu 24.

Hii ni mara ya kwanza Kenya kushiriki mashindano haya ya kombe la dunia kwa wachezaji wa kandanda ya walemavu. Kocha Morris Shikanda anasema matumaini yao ni haba.

''Haja yetu kubwa ni kupata ujuzi katika mashindano hayo, sisi hatuna ujuzi kama Ghana lakini ni jambo la maana sana kushiriki. Tunaomba serikali na wahifadhi wengine watusaidie,’’ asema Shikanda.

Image caption Kenya na Ghana ndizo nchi pekee zitakasohiriki kutoka Afrika

Nahodha wa timu ya Kenya Ibrahim Wafula anasema walifuzu kwa kombe la dunia wakati wa mashindano ya kombe la mataifa ya Afrika nchini Liberia mwaka jana mwezi Disemba, na kwamba tofauti na timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars ambao walisafiri Brazil kutizama kombe la dunia wao watakua uwanjani.

''Sisi tutacheza, na tunajivunia hilo licha ya ulemavu wetu tumekua timu ya kwanza Afrika Mashariki kucheza kwenye kombe la dunia. Hatuendi Mexico kama watazamaji jinsi walivyofanya Harambee Stars,’’ asema Wafula.

Mwandishi wa michezo wa BBC John Nene anasema Liberia na Ghana ni miongoni mwa mataifa hodari barani Afrika kwenye kandanda ya walemavu.

Mmoja ya wachezaji wa Kenya Dedan Ireri, ambaye anafanya kazi ya uchuuzi, asema anafurahishwa na maendeleo ya mchezo huu Afrika licha ya matatizo yanayowakumba nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa jumla.

Liberia na Sierra Leone yamejiondoa kwa sababu ya ugonjwa wa Ebola nchini humo.