Mkuu wa QPR aomba radhi

Haki miliki ya picha All Sport
Image caption Meneja wa timu amewataka mashabiki kuwawia radhi

Mwenyekiti wa QPR ameomba msamaha kwa misuko suko inayoshuhudiwa katika klabu hiyo.

Tony Fernandes amewaamrisha kiungo wa kati Adel Taarabt na meneja wa klabu hiyo Harry Redknapp kusuluhisha tofauti zao.

Katka taarifa yake , Fernandes amesema wawili hao wameleta aibu kwa kuvutana kuhusu uzani wa Taarabt na kuomba msamaha kwa mashabiki kwa tabia yao.

"Nimeongea nao mimi binafsi," Fernandes alifichua.

"Wote wawili wamejulishwa kuhusu masikitiko tuliyonayo kutokana na vitendo vyao."

"Kwa sasa macho yetu tumeyaelekeza kwa mechi ijayo dhidi ya Aston villa iliyoratibiwa kuchezwa hapo jumatatu, ingawa siku za hivi karibuni tumekuwa na wakati mgumu, tunatumai tutaweza kugeuza udhaifu wetu kuwa nguvu yetu na hivyo kuonyesha ustadi wa hali ya juu kuliko ilivyokuwa jumapili iliyopita," taarifa hiyo ilisema.

Katika vuta ni kuvute iliyoanza baada ya timu ya QPR kushindwa na Liverpool mabao 3-2 hapo jumapili, meneja Redknapp alimtaja mchezaji Taarabt kama "mchezaji mwenye tajriba kubwa lakini mbaya zaidi kuwahi kukutana naye".