Uhaba wa fedha kuathiri mechi za Malawi

Image caption Malawi National Team

Malawi imetangaza kuwa huenda ikashindwa kushiriki katika mechi za kufuzu kwa dimba la bara afrika mwaka 2015 kwa kuwa haina fedha za kucheza mechi zake mbili za mwisho.

Kufikia sasa Malawi iko katika nafasi ya tatu katika kundi Ba ikitarajiwa kucheza na Mali na Ethiopia.

Katibu mkuu wa Shrikisho la soka nchini Malawi Suzgyo Nyirenda ameiambia BBC kwamba wanajaribu kutafuta mfadhili ili kugharamia maandalizi ya mechi hizo.

Hatahivyo amesema kuwa uamuzi kamili utatolewa kati tarehe 4 na 5 mwezi Novemba.

Malawi inatarjiwa kucheza na Mali nyumbani tarehe 15 mwezi Novemba kabla ya kusafiri hadi Ethiopia siku nne baadaye.

Iwapo watashindwa kupata fedha za kusimamia mechi hizo,wataondolewa katika michuano hiyo hatua itakayoathiri nafasi yao ulimwenguni.

Malawi imepata ushindi dhidi ya Ethiopia lakini ikapoteza dhidi ya Mali.

Iwapo matokeo hayo yatatupiliwa mbali basi ,itamaanisha kwamba Ethiopia na Mali zitakuwa na alama sawa na kupigania nafasi ya pili kufuzu nyuma ya Algeria,ambao tayari wamefuzu.

Bwana Suzgyo amesema kuwa tayari serikali imewaeleza kwamba hawataweza kusimamia gharama za mechi hizo.

Timu hiyo inahitaji takriban dola 155,000 kumaliza mechi zake.