Corithians yawaenzi mashabiki wake

Haki miliki ya picha bb
Image caption Mashabiki wa timu ya Corithians ya Brazil wakiwa uwanjani kufuatilia mechi za timu hiyo.

Timu ya mpira wa miguu ya Corinthians nchini Brazil inatarajiwa kufungua eneo la makaburi kwa ajili ya mashabiki wake ambao wanataka kuzikwa karibu na wachezaji wao maarufu.

Mashabiki wataweza kuchagua vitalu hadi kufikia 70,000 katika eneo la "Corinthians Forever" yaani "Wakarintho Milele" karibu na jiji la Sao Paulo.

Eneo hilo pia litatumika kama mahali pa pumziko la milele kwa baadhi ya wachezaji maarufu wa timu hiyo.

Timu ya Corinthians ni ya pili kwa kuwa na wingi wa mashabiki wanaofikia milioni 25 nchini kote Brazil.

Eneo hilo la makaburi litakuwa na vyumba vya shughuli, bustani, mgahawa, ziwa na msitu wa hifadhi, amesema Ricardo Polito, afisa mtendaji mkuu wa kampuni inayosimamia mradi huo.

Image caption Shabiki wa timu ya Corithians ya Brazil akiomba dua kwa ajili ya timu yake.

Mashabiki wa timu ya Corinthian, wanaojiita"watiifu" - lakini wanajulikana na mashabiki wa timu pinzani kuwa"genge la vichaa"- kwa sasa watapata fursa ya kuendeleza ushabiki wao milele.

Waandishi wa habari wanasema mashabiki wa Corinthians wataungana na kundi dogo la klabu nyingine za mpira wa miguu ambazo zinatoa eneo la kuzika mashabiki, ikiwemo Boca Juniors kutoka Argentina.

Vitalu vya makaburi vitagharimu kati ya dola za Kimarekani $1,870 na $3,240) kutegemeana na eneo la makaburi lililochaguliwa na ukaribu wake na watu maarufu wa klabu hiyo ambao nao watazikwa hapo.

Wanaounga mkono hatua hiyo wanasema ni jambo jema kuwapa nafasi hiyo mashabiki wanaojulikana kwa moyo wa mapenzi kwa timu hiyo.

Mwezi uliopita, timu ya Corithians ilipewa onyo na mamlaka kwa kuitaka kuwazuia mashabiki wake kutotoa lugha ya matusi kwa timu pinzani, hususan wapinzani wa jadi timu ya Sao Paulo, ambayo mlinda mlango wake amekuwa akitukanwa.