Maelfu wamzika Meyiwa Afrika Kusini

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Marehemu Senzo Meyiwa, nahodha na mlinda mlango wa timu ya taifa ya Afrika Kusini.

Maelfu ya watu wamehudhuria mazishi ya aliyekuwa nahodha wa timu ya soka ya Afrika Kusini Senzo Meyiwa yanayofanyika jijini Durban.

Meyiwa, mwenye umri wa miaka 27, alipigwa risasi Jumapili iliyopita, baada ya majambazi kuingia nyumbani mwa mpenzi wake karibu na Johannesburg.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Senzo Meyiwa akiokoa mchomo katika moja ya mechi alizocheza wakati wa uhai wake.

Mtuhumiwa wa mauaji ya Meyiwa alifikishwa mahakamani Ijumaa na alishitakiwa kwa mauaji dhidi ya mlinda mlango huyo maarufu nchini Afrika Kusini.

Kifo cha Meyiwa kilisababisha mshituko mkubwa nchini Afrika Kusini na yameonyesha kiwango cha juu cha uahlifu wa kutumia nguvu nchini humo.

Mazishi yanafanyika katika uwanja wa mpira wa miguu wa Moses Mabhida Stadium katika mji wa Durban nyumbani kwa Meyiwa.

Senzo Meyiwa alionekana kama kivutio katika mchezo wa mpira miongoni mwa wananchi wa Afrika Kusini.

Image caption Jeneza la Senzo Meyiwa

Wengi wa waombolezaji wamevaa fulana zenye picha ya Meyiwa, mtu ambaye alikuwa kivutio kikubwa kimichezo.

Mazishi ya mwanamichezo mwingine shujaa wa Afrika Kusini, bingwa wa zamani wa dunia wa mbio za mita 800 Mbulaeni Mulaudzi, pia yatafanyika Jumamosi.

Mulaudzi aliuawa katika ajali ya gari kabla ya kifo cha Meyiwa.

Bendera nusu mlingoti

Rais Zuma ameamuru bendera ya taifa ipepee nusu mlingoti siku ya Jumamosi ili kumuenzi mlinda mlango huyo wa timu ya taifa.

Mechi kati ya timu za Orlando Pirates na Kaiser Chiefs katika ligi ya Afrika Kusini imeahirishwa baada ya kifo cha Meyiwa.

Image caption Rais Jacob Zuma akiwa na Senzo Meyiwa katika moja ya michezo ya timu ya taifa ya Afrika Kusini

Senzo Meyiwa alikuwa nahodha na mlinda mlango wa timu ya Afrika Kusini, Bafana Bafana.

Mamlaka ya soka nchini humo wametangaza mchezo wa timu ya taifa ya Afrika Kusini wa kufuzu fainali za kombe la mataifa ya Afrika dhidi ya Sudan ifanyike Durban.

Polisie wamesema Ijumaa kuwa mtuhumiwa wa mauaji ya Meyiwa alitambuliwa katika gwaride la utambuzi.

Mtuhumiwa huyo, Zanokuhle Mbatha, mwenye umri wa miaka 25, anakabiliwa na mashitaka ya mauaji na ujambazi wa kutumia silaha na anatarajiwa kufikishwa tena mbele ya mahakama Novemba 11.Polisi wametangaza zawadi kwa mtu atakayewezesha kupatikana kwa taarifa zaidi kuhusu shambulio hilo ili kuwanasa watuhumiwa wengine.