Ronaldo akana kumsema vibaya Messi

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Leonel Messi na Cristiano Ronaldo wanaelezwa kuwa hawapatani

Cristiano Ronaldo amekataa shutma kuwa amemsema vibaya kinara mwenzie katika kabumbu, Lionel Messi. kitabu kipya kuhusu mshambuliaji huyo wa Barcelona, kinaeleza kuwa mchezaji wa Real Madrid mara kwa mara amekuwa akitumia maneno ya kudhalilisha dhidi ya Messi.

Kumekuwa na tetesi kwa muda mrefu juu ya kutoelewana kwa Ronaldo na Messi.

Ronaldo amesema kuwa hizi ni habari za uongo na kusema kuwa atachukua hatua za kisheria kuwashtaki wanaohusika na usambazaji wa taarifa hizo.

Mchezaji huyo amejitetea kuwa anawaheshimu wachezaji wenzie wote, akiwemo Messi.

Ronaldo amemaliza ubabe wa Messi wa kutwaa tuzo ya Fifa ya mchezaji bora wa dunia kwa miaka mitatu mfululizo, Ballon d'Or baada ya kutwaa tuzo hiyo mwaka jana.

Zaidi ya yote wanandinga hao wametofautiana kwa goli moja tu ili kuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye ligi ya mabingwa barani Ulaya.Messi ana magoli 71 sawasawa na Raul Gonzales wakati Ronaldo ana magoli 70.

Messi anahitaji magoli mawili tu ili kuwa mfungaji bora wa muda wote wa ligi kuu ya Hispania-La Liga,amefunga magoli 250 katika michezo 285 nyuma ya Telmo Zarra wa Athletic Bilbao aliyecheza miaka ya 1940-1950.