Liverpool yaicharaza Leicester 3-1

Image caption Steven Gerrard akishangilia goli na wachezaji wenzake wa timu ya Liverpool, walipowalaza Leicester 3-1

Ligi ya kuu ya England iliendelea jana usiku katika viwanja mbali mbali. Leicester inayoburuza mkia katika ligi hiyo ikiwa na pointi 10 katika michezo 14 iliyocheza waliikaribisha Liverpool ambayo iliibuka na u

shindi wa magoli 3-1 katika mechi hiyo. Hadi kumalizikakwa kipindi cha kwanza timu hizo zilikuwa zimefungana goli 1-1. Kwa matokeo hayo Liverpool imeshika nafasi ya 8 nyuma ya Asernal , zote zikiwa na pointi 20. Hata hivyo Asernal imecheza mchezo mmoja pungufu ya Liverpool yenye mechi 14 ilizokwishacheza.

Matokeo mengine katika mechi za Jumanne usiku, Manchester United wakiwa kwenye uwanja wao wa Old Trafford, wameicharaza Stoke City mabao 2-1. Burnley imetoka sare ya kufungana bao 1-1 na Newcastle, Swansea wameitandika QPR magoli 2-0, Crystal Palace wamepoteza katika uwanja wao kwa kucharazwa goli 1-0 na Aston Villa. Nayo West Brom imepoteza kwa kufungwa 2-1 na West Ham.

Katika mechi za leo usiku, Arsenal watapepetana na Southampton katika uwanja wa Emirates, Chelsea vinara wa ligi watakuwa wenyeji wa Tottenham, huku Everton wakiikaribisha Hull City. Na Machester City inayoshika nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 27 watataka kujiimarisha na kupunguza pengo la pointi sita kati yake na Chelsea, pale watakapomenyana na wenyeji wao Sunderland.