Rais Kikwete amfuta kazi Tibaijuka

Image caption Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete ametengua nafasi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kupitia hotuba aliyotoa kuzungumzia kashfa ya upotevu wa fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.

Hatua hiyo imechukuliwa na Rais Kikwete mbele ya wazee wa Dar Es Salaam aliokuwa akiongea nao na matangazo kurushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya taifa na vyombo vingine.

Uchunguzi uliofanywa na kamati ya hesabu za umma ya Tanzania (PAC), ilidai kuwa Profesa Tibaijuka ni mmoja wa watu walionufaika kinyume cha sheria kwa kupata fedha zilizotoka katika akauti hiyo iliyofunguliwa kutunza fedha kusubiri ufumbuzi wa mgogoro wa kibiashara kati ya kampuni ya kusambaza umeme TANESCO na kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL.

Siku chache zilizopita Profesa Tibaijuja aliitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam kubainisha kuwa hakuwa akikusudia kujiuzulu kutokana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Hata hivyo Rais Kikwete hakutangaza kuwachukulia hatua watumishi wengine waliodaiwa kuhusika na tuhuma hiyo kwa maelezo kuwa uchunguzi zaidi unatakiwa kwa kila mtuhumiwa.

Kumekuwa na ubishi mkubwa kujadili endapo fedha ambazo ni mabilioni zilizochukuliwa zilikuwa za umma au la. Na hata Rais Kikwete amesema maelezo aliyopewa na wataalam yanaonyesha hazikuwa mali ya TANESCO.