Vipigo kutoka Kenya,ni somo:Tanzania

Image caption Timu ya Kriketi ya Tanzania

Kocha wa timu ya taifa ya kriketi Tanzania Hamisi Abdallah amesema kipigo ilichokipata timu yake hivi karibuni kutoka kwa timu za Kenya na Uganda kimempa somo na kujifunza makosa ili kujiweka tayari na mechi za kufuzu kombe la Dunia kwa timu za Vijana (Under-19) zitakazo fanyika mapema February mwakani huko Namibia.

Timu za Kenya A, Kenya B, Uganda na Tanzania hivi karibuni zilishindana huko Nairobi, Kenya kwa juma moja katika mechi michuano ya kirafiki ya kujipima nguvu ili kujiweka tayari kwa michuano hiyo ya kufuzu Kucheza kombe la dunia hapo mwakani.

“Michuano ilikuwa migumu, tuliweza kuwafunga Kenya A, tukafungwa na Kenya B na baadaye kufungwa na Uganda”.

“Bado tuna makosa madogo madogo katika kubeti na ku-field, baada ya mapumziko ya Krismas, tutaanza tena mazoezi ili kurekebisha makosa”, Alisema Abdalla, ambaye timu yake imerejea jana Dar es Salaam kutoka Nairobi.

Katika mechi ya mshindi wa tatu, Uganda waliifunga Tanzania kwa wiketi 9 huku wenjeji, Kenya A wakiwafunga Kenya B kwa mikimbio 65 na kuwa mabingwa.

“Tunahitaji kucheza mechi nyingi za majaribio ili kujiweka tayari na michuano ya kufuzu ili tuweze kucheza kombe la dunia kwa mara ya kwanza ili tuweke historia”, alisema Abdallah, aliyewahi kucheza kriketi ligi daraja la pili huko Uingereza katika klabu ya Watford Town.

Tanzania imefanikiwa kucheza mechi za kufuzu kucheza kombe la dunia baada ya kushinda michuano ya Afrika Daraja la Pili yaliyofanyika hivi karibuni huko Lusaka, Zambia katika michuano iliyoshirikisha timu za wachezaji wenye umri chini ya miaka 19 kutoka Zambia, Ghana, Swaziland Rwanda na Msumbiji.