Droo kupanga mechi kombe la FA yafanyika

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mabingwa watetezi wa kombe la FA, wakishangilia ushindi mwaka uliopita.

Droo ya kupanga mechi za raundi ya 4 ya Kombe la FA imefanyika.

Katika mpangilio huo, vigogo Manchester United imepangwa kucheza na timu ya daraja la chini ya Cambridge United.

Mabingwa Watetezi, Arsenal, watakuwa Ugenini kucheza na Brighton au Hove Albion ambayo ipo Daraja la chini ya Ligi Kuu England.

Chelsea itakipiga na Mill wall au Bradford City. Manchester City itapepetana na Middlesbrough

Southampton/Ipswich na Crystal Palace

Blackburn Rovers na Swansea City

Michezo ya raundi ya nne inatarajiwa kupigwa Januari 24 na 25.

NAKO kwenye kombe la mapinduzi

Baada ya kutojulikana kuwa nani atacheza na Simba katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Mapinduzi, sasa kila kitu kiko wazi. Simba itaivaa Taifa Jang'ombe katika mechi ya michuano hiyo hatua ya robo fainali hii leo usiku.

Mechi hiyo itachezwa saa 2 usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Siku inayofuata Alhamisi, mechi nyingine ya robo fainali itapigwa jioni, nayo ni kati ya Azam dhidi ya Mtibwa Sugar.

Mechi hiyo inaaminika kuwa moja ya zile ngumu na safi za michuano ya Mapinduzi.

Yanga sasa itacheza mechi yake ya robo fainali dhidi ya maafande wa JKU.

Mechi hiyo itapigwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Yanga inakutana na JKU baada ya kumaliza vinara wa kundi A wakiwa na pointi 9. Walipata pointi hizo baada ya kushinda mechi zote tatu katika makundi kwa kujikusanyia mabao tisa, wakiwa hawajafungwa hata moja.

Walikamilisha pointi hizo tisa baada ya kuifunga Shaba kwa bao 1-0 katika mechi tamu na ya kuvutia jana usiku.

Bao la mchezo huo lilifungwa na Mbrazil Andrey Coutinho.