Nahodha kriketi Tanzania aomboleza

Image caption Timu ya criket ya Tanzania

Nahodha wa timu ya taifa ya kriketi Tanzania, Hamis Abdallah amesema pengo la mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Enjo Seti( wa nne kutoka kulia katika picha mwenye miwani) aliyefariki dunia hivi karibuni kwa ugonjwa wa moyo halitazibika.

Seti, kwa mujibu wa watu wa karibu alifariki dunia Ijumaa akiwa matembezini baada ya kuugua ghafla.

"Kwa niaba ya wachezaji wenzagu, tumehuzunishwa na kifo cha mchezaji mwenzetu, tuliyeanza naye kujifunza kriketi katika miaka ya 1990 tukiwa bado vijana wadogo", alisema Abdallah.

“Tutamkumbuka sana Seti kwa ukarimu wake, ucheshi na upendo kwa wachezaji wenzake”, alisema Abdallah aliyewahi kucheza kriketi katika klabu ya Watford Town ya Uingereza miaka ya nyuma.

Seti, alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioshiriki michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Ligi ya Dunia Daraja la 4. Pia alisafiri na timu mwaka 2009 kwenda Uingereza chini ya mualiko ya klabu ya MCC ya nchini humo kwa ajili ya mazoezi na mechi za majaribio za timu ya taifa.