Kivumbi leo AFCON,Wababe dimbani

Haki miliki ya picha
Image caption Wababe kutoana kijasho

Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Itaendelea kutimua vumbi nchini Guinea ya Ikweta, ambapo timu za kundi D zitashuka dimbani kuwania pointi tatu muhimu.

Mchezo wa kwanza utawakutanisha Tembo wa Afrika Ivory Coast watakaokipiga na Guinea mchezo utakaochezwa Estadio De Malabo katika mji wa Malabo.

Kiungo wa Ivory Coast Yaya toure ambaye alikua majeruhi anatarajiwa kucheza mchezo huo baada ya Kocha wake Herve Renard kueleza kuwa Yaya anaendelea vizuri.

Timu hizi zimekutana mara 15 katika michezo rasmi huku Guinea ikipoteza michezo 10,ikishinda michezo mitatu na kutoka suluhu michezo miwili.

Mchezo mwingine utakua ni kati ya Mali na Cameroon ambao nao utapigwa Estadio de Malabo

Cameroon wanatarajia kumtumia nahodha wake Stephane Mbia ambae alikua anatumikia adhabu toka mwezi Novemba alikotolewa kwenye mchezo dhidi ya Ivory Coast.

Mali itamkosa mshambuliaji wake Cheick Diabate ambae alifanyiwa upasuaji mapema Mwezi huu, huku kiungo wa Mali Seydou Keita akijiandaa kucheza michuano hiyo kwa mara ya saba katika kipindi chake cha uchezaji.