AFCON:Congo:B yaibwaga Gabon 1-0

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Hii ni mechi ya kwanza kwa Congo Brazaville kushinda katika michuano ya AFCON tangu mwaka 1974

Tukiendelea kukuletea taarifa za michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, yanayoendelea nchini Equatorial Guinea, jana usiku Congo Brazaville iliweza kupata pointi tatu muhimu baada ya kuibwaga Gabon bao 1-0.

Katika mzunguko wa kwanza Congo ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji Equatorial Guinea, huku Gabon ikiicharaza Burkina Faso mabao 2-0. Congo imepata ushindi wake wa kwanza katika michauno ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu fainali za mwaka 1974.

Bao la Congo lilipatikana katika dakika ya 48 likifungwa na Oniangué. Congo ndiyo inayoongoza kundi A kwa kuwa na pointi 4 ikifuatiwa na Gabon yenye pointi 3, wenyeji Equatorial Guinea wakiwa katika nafasi ya tatu na pointi mbili. Mwisho ni Burkina Faso yenye pointi 1, baada ya jana kutoka sare ya kutofungana na wenyeji Equatorial Guinea katika mzunguko wa pili wa kundi A.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Kocha Claude LeRoy alichukua usukani katika michuano yake ya 34 ya AFCON

Katika mchezo wa mapema wa kundi hili, Equatorial Guinea na Burkina Faso zimeshindwa kutambiana baada ya kukamilisha dakika 90 za mchezo zikiwa hazijafungana na hivyo kugawana pointi moja moja.

Sare yoyote na Burkina Faso Jumapili katika mzunguko wa tatu wa kundi A utaiwezesha Congo kufuzu kucheza hatua ya robo fainali. Kadhalika atakayeshinda kati ya Gabon na Equatorial Guinea katika mchezo wa Jumapili huko Bata, pia atafuzukuingia katika hatua ya timu nane yaani robo fainali.

Leo usiku ni mtifuano wa timu za kundi B, ambapo mchezo wa kwanza utazikutanisha Zambia na Tunisia na baadaye Cape Verde na DR Congo.

Timu za kundi hili zote zina pointi moja moja.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Levy Madinda alikuwa tisho kubwa kwa Gabon ingawa alikosa nafasi nyingi za kuingiza mabao