Chaneta Tanzania kukutana na Serikali

Image caption Mchezo wa netball ukichezwa

Chama cha mchezo wa pete (netball) nchini Tanzania (Chaneta) kimepanga kukutana na serikali kujadili namna ya kuandaa mashindano ya Afrika yatakayofanyika kati kati ya mwezi huu nchini.

Chaneta, kwa mujibu wa kiongozi wake, Anna Kibira kimepewa nafasi ya kuandaa michuano hiyo mikubwa na shirikisho la mchezo huo duniani (INF).

Tanzania imepata nafasi ya kuandaa baada ya taarifa kueleza kuwa Zambia, ambayo ndio ilichaguliwa kuandaa hapo awali, kutokuwa tayari kufanya hivyo.

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Tanzania kuandaa michuano mikubwa ya mchezo wa pete ukiachilia mbali mashindano ya Afrika ya Mashariki ambayo imekuwa ikiandaa mara kwa mara huku timu kutoka Kenya, Uganda, Zanzibar zikishiriki.

Miaka michache kadhaa iliyopita, Tanzania ilifanikiwa kuandaa michuano ya kombe la Mataifa (Nations Cup) iliyofanyika uwanja wa Taifa.

Michuano hiyo ndiyo iliifanya Tanzania kuingia katika viwango vya dunia vya INF na ilifanikiwa kushinda kombe hilo (Nations Cup) baada ya kualikwa kushiriki nchini Singapore.

Tanzania kwa sasa, kwa mujibu wa viwango vya dunia ya INF vilivyotolewa mwezi December mwaka jana, ipo katika nafasi ya 15 katika ngazi ya dunia na ipo nafasi ya 4 katika Afrika baada ya Malawi, Afrika ya Kusini, Uganda, ambayo kwa sasa ndio mabingwa wa Nations Cup na ikifuatiwa na Tanzania.

Kwa mujibu wa Kibira, Chaneta ina mipango ya kuifanya timu ya Taifa, Taifa Queens kushiriki michuano mingi ili kujiandaa na michuano mbalimbali ya kimataifa, baada ya mwaka jana kushindwa kushiriki michuano mbalimbali kama vile ya kufuzu kombe la dunia kutokana na ukata (ukosefu wa fedha).