Kriketi Vijana:Tanzania,Namibia kuchuana

Image caption Mcheza Kriketi akiwa mazoezini

Wenyeji Tanzania watacheza na Namibia katika mechi ya ufunguzi ya Ligi ya Kriketi ya Afrika kwa vijana wa kiume wenye umri chini ya miaka 19 itakayochezwa katika uwanja wa Gymkhana jijini Dar es Salaam Jumamosi ya February 14.

Wachezaji wa Tanzania wanafanya mazoezi Dar es Salaam wakiwa chini ya kocha mchezaji, Hamis Abdallah.

Michuano hiyo ya Juma moja itakuwa ni sehemu ya kufuzu kucheza kombe la dunia la vijana chini ya miaka 19 litakalofanyika, Dhaka, Bangladesh mwakani.

Timu nyingine Shiriki za michuno hiyo kufuzu zitatoka katika nchi za Namibia, Nigeria, Botswana, Kenya na Uganda na zinategemewa kuwasili Dar es Salaam siku mbili kabla ya mashindano.

Kocha Abdallah, aliyewahi kucheza kriketi katika Klabu ya Watford Town ya Uingereza kwa miaka kadhaa, amesema atachagua timu yake ya mwisho baada ya mechi za majaribio zitakazochezwa wikiendi hii.

''Kwa sasa nina kikosi (provisional squad) cha wachezaji zaidi ya 20 kambini, nitachagua timu ya wachezaji 12 ambao ndio watakuwa wawakilishi wa Tanzania katika michuano hiyo”, amesema Abdalllah, aliyesomea ukocha na ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa ya wakubwa.