Kilimanjaro Marathon yanukia

Image caption Mkimbiaji kutoka nchini Kenya

Wakimbiaji mashuhuri kutoka Kenya, Uganda na kwingine barani Afrika, Ulaya, America na Asia ni miongoni mwa washiriki wanaotegemewa kuchuana katika mbio za kimataifa za Kilimanjaro Marathon siku ya Jumapili mkoani Kilimanjaro, Moshi, Kaskazini mwa Tanzania.

Kenya, moja ya nchi maarufu kwa mchezo wa riadha duniani imekuwa ikishiriki mara nyingi tangu mbio hizo zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kuanzishwa mwaka 2003.

Wanariadha wa Kenya walitawala mbio za mwaka jana ambapo katika mbio ndefu (full marathon-wanaume), nafasi sita za juu zilishikwa na Wakenya huku David Rutoh-akiwa namba moja na kumaliza mbio kwa muda wa 2:16:06.

Kwa upande wa wanawake (full marathon), Kenya pia ilishika nane nae za juu, mshindi wa kwanza akiwa ni Fridah Lodepa akishinda kwa muda wa 2:40:26 huku Joan Rojich akimaliza wa pili katika muda wa 2:44:24

Wenyeji Tanzania imekuwa ikishinda katika mbio ndefu miaka ya nyuma na katika mbio za hivi karibuni ikitawala katika Nusu Marathon (half marathon).

Kwa mujibu wa waandaaji, Wild Frontiers, zaidi ya wanariadha 6000 wanategemewa kushiriki wakiwemo wa kigeni kutoka nchi mbalimbali Afrika, Ulaya, America na Asia

Mbio hizo, zinazofanyika kila mwaka, zimekuwa zikitoa fursa kwa wakimbiaji wageni kuuona mlima mrefu kuliko wote barani Afrika, Mlima Kilimanjaro, ikiwa ni kama sehemu ya kuendeleza na kukuza utalii wa ndani ya nchi.

Katika msimu wa Kilimanjaro Marathon, mji wa Moshi hufurika wageni wengi na wenyeji kujiingia kipato kutokana na kufurika kwa watu katika hoteli, hivyo mkoa kujipatia fedha za kigeni.