Suarez aiadhibu Man City UEFA

Haki miliki ya picha AP
Image caption Luis Suarez

Mshambuliaji wa Zamani wa Liverpool Luis Suarez amerejea nchini England hapo jana na bahati ya kipekee baada ya kuiwezesha timu yake mpya ya Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao mawili 2 kwa moja dhidi ya wapinzani wao Manchester City katika mechi ya Klabu Bingwa barani Ulaya .

Suarez aliwashangaza mashabiki wa Man City baada kupachika wavuni mabao yote mawili na hivyo kuwaonyesha ni moto wa kuotea mbali anapofika kwenye kisanduku cha kumi nane.

Goli pekee la kufutia machozi la Manchester City lilitiwa kimiani na mshambuliaji wa timu hiyo Sergio Aguero. Na hivyo hadi mechi hiyo inamalizikia Man City wakiwa nyumbani walijikuta wakivuna juani goli moja dhidi ya magoli mawali ya Barcelona.

Na katika mechi nyingine ya michuano hiyo Juventus ya Italia wakiwa nyumbani waliwaadhibu Borussia Dortmund ya Ujerumani baada ya kuwashushia kichapo cha magoli mawili kwa moja.

Magoli ya Juventus yalitiwa kimiani na Carlos Tevez na Alvaro Morata huku lile la Borussia Dortmund likitiwa kimiani na Marco Reus.

Kindumbwe ndumbe cha michuano hiyo kitaendelea tena hii leo ambapo Arsenal ya England watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Monaco ya Ufaransa huku Bayern Levekuzen wakimenyana vikali na Altetico Madrid ya Hispania. Mechi hizo zote zitapigwa mwendo wa saa 4:45 kwa saa za Afrika Mashariki.