FIFA:Hakuna fidia ya kombe la dunia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Jerome Valcke

Shirika la kandanda duniani FIFA, limetangaza kuwa halitazilipa fidia klabu zozote za soka barani Ulaya ambazo hazijafurahia hatua ya FIFA kuandaa kombe la dunia nchini Qatar mwezi Novemba na Disemba ya mwaka wa 2022.

Katibu mkuu wa shirikisho hilo, Jerome Valcke, amesema kuwa FIFA haina haja ya msamaha wowote wa maandalizi ya uwenyeji wa mashindano hayo, ambayo yanatazamia kutatiza pakubwa ratiba ya michuano ya ligi kuu barani Ulaya.

Hapo jana mapendekezo ya jopo la FIFA yalisema kuwa mashindano ya kombe hilo la dunia nchini Qatar yatafanyika wakati wa baridi ili kuepuka msimu wa kiangazi katika mataifa ya ghuba ambayo hushuhudia joto kali mno.