Cisse,Evans wapewa muda kujitetea

Image caption Papiss Cisse na Johny Evans wanashutumiwa kutemeana mate uwanjani

Mchezaji wa Newcastle United Papiss Cisse na Johny Evans wa Manchester United wanashitakiwa na chama cha soka England FA kwa kosa la kutemeana mate. Cisse mwenye umri wa miaka 29, aliomba radhi kwa upande wake kwa tukio hilo lililotokea katika mchezo wao uliomalizika kwa matokeo ya ushindi wa bao moja kwa bila waliopata mashetani wekundu siku ya Jumatano.

Mlinzi Evans wa Manchester amekana kumtemea mate Cisse kwa makusudi.

Jopo la waamuzi watatu wa zamani waliziangalia picha za video Alhamisi na kukubaliana kuwa wachezaji hao walitakiwa kutolewa nje ya uwanja kutokana na kitendo hicho, jambo ambalo limekifanya chama cha FA kuwafungulia mashitaka.

Wachezaji wote wawili wanakabiliwa na adhabu ya kufungiwa michezo sita kila mmoja kama watakutwa na makosa na wamepewa muda mpaka saa tatu usiku Ijumaa leo hii kuweza kujitetea. Ilikuwa ni dakika ya 38 ya mchezo huo pale wachezaji hao walipotemeana mate. Lakini wasimamizi wa mcheozo huo hawakuona kitendo hicho na ilibainika kwa kutumia picha za video

Mashabiki wa soka wa England na sehemu nyingine za dunia, watashuhudia kitimtimu cha mechi za FA weekend hii kwa michezo kadhaa kupigwa. Siku ya Jumamosi, Aston Villa watawakaribisha West Brom, huku Bradford wakipepetana na Reading. Siku ya Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu ambao utaihusisha Liverpool watakapokuwa nymbani kuvaana na Blackburn.