Mwanariadha wa S Leone akamatwa UK

Image caption Wanariadha wa Sierra Leone

Mwanariadha wa mbio fupi kutoka Sierra Leone ambaye amekuwa akilala katika barabara za mji wa Uingereza huenda akafukuzwa nchini humo baada ya kukamatwa.

Jimmy Thoronka mwenye umri wa miaka 20 alikuwa tegemeo la taifa lake katika mbio za mita 100 lakini hakurudi nyumbani Afrika baada ya mashindano ya jumuiya ya madola mjini Glasgow kukamilika mwaka uliopita kufuatia hofu ya Ebola.

Thoronka ambaye alikuwa hana makaazi anasema Ebola imewaua familia yake nchini Sierra Leone.

Polisi wa MET wanasema mwanariadha huyo alikamatwa siku ya ijumaa kwa kukiuka sheria za uhamiaji na sasa anazuiliwa na kikosi cha polisi wa mpakani.

Ndoto za Jimmy kuwa mmoja ya wanariadha maarufu duniani itafaulu tu iwapo ataendelea kuishi nchini Uingereza na kupata mtu wa kufadhili mazoezi yake.

Abdul Karim Sessay mmoja ya wasemaji wa shirikisho la riadha nchini Sierra Leone amesema kuwa hawawezi kuzungumzia kesi za watu binafsi ,lakini kuna usaidizi kwa watu kurudi nyumbani iwapo hawastahili kusalia nchini Uingereza.

Thoronka amesema kuwa hawezi kurudi Sierra Leone kwa kuwa hawezi kuishi huko pekee hivyobasi aliishi na marafikize mjini Leicester kabla ya kuelekea London.