Pambano la watani wa jadi,Simba kidedea

Image caption Okwi, wa tatu kutoka kulia akishangilia.

Goli lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi lilitosha kuipa Simba ushindi wa 1-0 dhidi ya mahasimu wao, Yanga katika mechi ya watani wa jadi ( Dar es Salaam derby),Ligi kuu Tanzania, iliyochezwa katika uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Zaidi ya mashabiki 57,000 walihudhuria mechi hiyo, wakiwa wamevalia nguo za rangi ya njano (inayoiwakilisha Yanga) na rangi nyekundu ( inayoiwakilisha Simba.

Okwi alifunga goli hilo dakika 52 kwa umbali usiopungua mita 23 baada ya kipa wa Yanga, Ali Mustapha “Barthez” kupiga hesabu fyongo ( kuutuokea mpira).

Mpira ulimpita juu Barthez na kuingia golini ukimwacha umbali wa zaidi mita tatu akiutazama.

Yanga walibaki wachezaji 10 uwanjani (dakika ya 74) baada ya mshambuliaji wake, Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda kupiga mpira wavuni licha ya refa kupiga filimbi ilihali akiwa na kadi ya njano aliyopewa hapo awali.

Yanga, licha ya kipigo, inabaki kileleni ikiwa na pointi 31, huku Azam FC wakiwa na pointi 30 na Simba imefikisha pointi 26.