Chamberlain kukaa nje mwezi mmoja

Image caption Alex Oxlade-Chamberlain hatokuwepo kwa mwezi mmoja

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger atalazimika kujikuna kichwa baada ya kupata habari kuwa kiungo chake cha kutegemewa Alex Oxlade-

Chamberlainhatakuwepo kwa takriban majuma tatu hadi nne zijazo kutokana na jeraha nyuma ya goti.

Kulingana na kocha huyo,Chamberlain alipata jeraha hilo katika mechi ya kukata na shoka ya FA dhidi ya wapinzani wao wa jadi Manchester United jumatatu iliyopita.

Kujeruhiwa kwake ni pigo kwa azimio la Arsenal kuimarisha matokeo yao katika ligi kuu ya Uingereza ambapo sasa wanashikilia nafasi ya tatu .

Haki miliki ya picha PA
Image caption Alex Oxlade-Chamberlain alichangia pakubwa katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Manchester united katika FA

Aidha Arsenal wanajiandaa kwa mechi ya marudio ya mkondo wa 16 bora katika ligi kuu ya mabingwa barani Ulaya ambapo wameratibiwa kuchuana dhidi ya Monaco juma lijalo.

Winga huyo alikuwa amerejea mwishoni mwa mwezi Februari baada ya kukaa mwezi mmoja nje kufuata jeraha lengine la kiuno.

Wenger hata hivyo alipata afueni katika safu ya ulinzi baada ya kurejea kwa Gabriel aliyejeruhiwa katika mechi ngumu dhidi ya QPR mnamo Machi tarehe 4.