Arsenal washindwa kusonga Ulaya

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Arsenal vs Monaco

Pamoja na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 wakiwa ugenini katika mchezo uliopigwa usiku wa kuamkia leo, washika bunduki wa jiji la London Arsenal wameshindwa kusonga mbele katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya kwa kosa la kuruhusu magoli mengi wakiwa nyumbani katika mchezo wa awali, ambapo Monaco iliwabamiza wenyeji wao hao Arsenal kwa jumla ya mabao 3-1.

Arsenal ilijipatia goli la kwanza dakika ya 36 ya mchezo huo kupitia mchezaji wake Olivier Giroud kabla ya Aaron Ramsey kuongeza la pili katika dakika ya 79 ya mchezo huo. Matokeo ya jumla kwa timu hizo ni 3-3 japo Monaco inasonga mbele kwa faida ya kuwa na magoli mengi ya ugenini na kuwaacha vijana wa mzee Wenga wakikosa kufika robo fainali kwa mara ya tano mfululizo. Kitimtimu hicho cha klabu bingwa Ulaya kilitimua vumbi pia huko nchini Hispania pale, Atletico Madrid ilipowakaribisha Bayer Leverkusen kutoka Ujerumani. Katika mchezo huo wenyeji Atletico wamefanikiwa kusonga mbele kwa mikwaju ya Penati baada kumaliza dakika 120 wakiwa mbele kwa bao moja ambalo halikutosha kuamua mshindi kutokana na matokeo ya mchezo wa awali ambapo Leverkusen iliibanjua Atletico bao moja kwa bila. Wakiwa mbele ya mashabiki wao lukuki Atletico ilishinda penati 3 dhidi ya 2 za wageni wao na kutinga moja kwa moja katika hatua ya robo fainali wakiungana na ndugu zao Real Madri. Ligi hiyo itaendelea tena leo hii kwa michezo miwili kupigwa. Borussia Dortmund watavaana na Juventus huku miamba ya soka ya Hispania Barcelona ikiialika Manchester City kutoka England.