Matumla Junior kumvaa Hua

Kuna msemo usemao “Mtoto wa nyoka ni nyoka” na msemo huu unajidhihirisha katika mpambano kati ya mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia wa WBU, Rashid Matumla, Mohamed atakapozichapa na bondia kutoka China, Wang Xiu Hua katika pambano la ubingwa wa WBF la uzani wa Super Bantam siku ya Jumamosi jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

Hua tayari amewasili nchini Tanzania na Mohamed amesema amejiandaa vya kutosha kushinda mbele ya mashabiki wa nyumbani.

Kwa mujibu wa waandaaji, mshindi kati ya Matumla Junior na Hua atapata nafasi ya kucheza katika moja ya mapambano ya utangulizi (supporting cards) katika pambano la bondia Floyd Mayweather na Pacquiao litakalochezwa Mei 2 jijini Las Vegas.

Watu kadhaa mashuhuri wanategemewa kuangalia pambano la Matumla Junior na Hua akiwemo bondia wa zamani wa uzito wa juu wa Afrika ya Kusini, Francois Botha, aliyewahi kupingana na bingwa wa zamani, Mike Tyson na Evander Holyfield katika enzi zake.