Shirikisho la ngumi Tanzania lina ukata.

Image caption Mabondia wa Tanzania

Licha ya kuchagua timu ya taifa , Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) halina fedha kwa ajili ya kuigharamia timu hiyo kusafiri kwenda nchini Congo Brazzaville kwa ajili ya kushiriki michezo ya Afrika (All Africa Games ) itakayofanyika mwezi Septemba na badala yake, shirikisho hilo limesema linaitegemea serikali kusaidia gharama hizo.

Uongozi wa BFT umesema una imani serikali itagharamia wachezaji kwa ajili ya michezo hiyo, kufuatia ahadi iliyoweka hapo awali.

Katibu mkuu wa BFT, Makore Mashaga amesema wao wamechagua wachezaji 10 lakini ushiriki wao utategemea na uwezo wa serikali, ambayo licha ya wachezaji wa ngumi, pia inategemewa kugharamia wachezaji wa michezo mingine kama vile riadha, judo, kuogelea na mpira wa meza (table tennis) kuelekea michezo hiyo.

Serikali iligharamia wanamichezo wa michezo mbalimbali wa Tanzania kufanya mazoezi nje ya nchi wakati wa maandalizi ya michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Glasgow na kusema kuwa licha ya kufanya vibaya michuano hiyo, ina angalia uwezekano wa kuwasaidia tena wanamichezo hao katika michezo ya Afrika ili wafanye vizuri kuliwakilisha taifa.

Wanamichezo wa Tanzania, licha ya kuwe na vipaji na uwezo, wamekuwa wakifanya vibaya katika michezo mingi ya kimataifa kwa ukosefu wa fedha kwa ajili ya mazoezi ya muda mrefu na kushindwa kucheza michezo ya majaribio ndani na nje ya nchi.