Shepolopolo kutua Dar kuikabili Twiga

Image caption Timu ya Taifa ya Zambia Shepolopolo itakayo kipiga na timu ya taifa ya Tanzania Twiga stars

Timu ya soka ya taifa ya wanawake ya Zambia (Shepolopolo) inatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Jumatano kwa ajili ya mechi yake ya marudiano na wapinzani wao Tanzania (Twiga Stars) ili kugombania nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika mwaka huu inayotarajiwa kufanyika Congo Brazzaville kuanzia Septemba 4-9.

Twiga Stars iliifunga Shepolopolo mabao 4-2 katika mechi ya kwanza iliyochezwa Nkoloma jijini Lusaka nchini Zambia na endapo timu hiyo, chini ya kocha Rogasian Kaijage itashinda tena mechi ya nyumbani, basi itakuwa imefuzu kwa ajili ya fainali hizo.

Mechi hiyo ya marudiano itachezwa siku ya Ijumaa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kama ilivyo ada, Wazambia hao watapata nafasi ya kufanya mazoezi katika uwanja huo kabla ya mechi ili kuuzoea na kujiweka fiti mara ya mwisho kabla ya mechi.

Hata hivyo,kocha wa Shepolopolo Albert Kachinga naye anahitaji ushindi licha ya kufungwa nyumbani akiwa amerekebisha makosa kadhaa yaliyopelekea kufungwa.