Cecafa yatoa pole kwa mauaji ya Garissa

Image caption Wapiganaji wa kikundi cha Al Shabaab.

Baraza la Vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limeelezea masikitiko yake juu ya mauaji ya Chuo cha Garissa yaliyoua zaidi ya watu 147 nchini Kenya katika shambulio la kigaidi.

Meneja wa mawasiliano wa Cecafa, Rogers Mulindwa, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, amesema Cecafa imestushwa na kuipa pole Kenya kama sehemu ya baraza hilo.

Mulindwa amesema wajumbe wa baraza hilo walikaa kimya kwa muda wa dakika moja wakati wa mkutano wake mkuu nchini Cairo, Misri ikiwa kama ishara ya kuomboleza mauaji hayo.

Amesema wajumbe wa Cecafa wamepatwa na mstuko kutokana na tukio hilo ambalo limehusisha raia wasio na hatia, huku wakitoa wito wa kupambana na ugaidi na kumpa pole raisi wa Kenya, Uhuru Kenyatta na watu wake.

Kenya imekuwa ikishambuliwa na kikundi cha kigaidi cha Al-Shaabab kwa kile kinachodaiwa na kuhusika kwake kupeleka sehemu ya askari wake nchini Somalia kuungana na jeshi la Afrika katika jitihada za kuiokomboa nchi hiyo, ambayo ni ngome ya Al-Shaabab.