Sophia Mwasikili awasifu wenzake

Image caption Sofia Mwasikili mwenye rasta akiwaongoza wachezaji wa Twiga wakati wa mazoezi.

Nahodha wa timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini Tanzania , Sophia Mwasikili amewasifu wachezaji wenzake kwa kufuzu kucheza fainali za Michezo ya Afrika (All Africa Games) huku akitoa wito wa kujituma zaidi kwa ajili ya kufanya vizuri katika michuano hiyo ya Afrika.

Twiga Stars ya Tanzania imefuzu kucheza fainali za michezo hiyo itakayofanyika nchini Congo Brazzaville, Septemba mwaka huu baada ya kuwafunga Zambia (Shepolopolo) katika mechi ya marudiano ya kufuzu katika soka la wanawake iliyofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.“Tumeweza kuvuka hatua hii muhimu, huko tuendako ni kugumu zaidi hivyo inabidi tujiandae vizuri ili kutoa ushindani”, alisema Mwasikili.

Kufuzu kwa Twiga kunakuja licha ya kufungwa 3-2 katika mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .Kwa matokeo hayo, Twiga imefuzu kwa jumla ya mabao 6-5, kufuatia ushindi wake wa awali wa 4-2 ulioupata katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Lusaka.

Mabao ya Twiga yalifungwa na Asha Rashidi mapema dakika ya 3, huku Mwanahamisi Chiuwa akifunga goli la pili dakika ya 29 na kuongoza 2-0 hadi mapumziko.

Zambia ilipata goli dakika ya 5 baada ya kipindi cha pili kupitia Grace Chanda, Irene Lungu akifunga goli la pili dakika ya 61 na Misozi Chisa akifunga goli la tatu dakika ya 90.

Michuano hiyo ya Michezo ya Afrika itashirikisha timu katika michezo mbalimbali, ikishirikisha timu za Afrika.