Drogba arejesha alichojaaliwa kwa jamii.

Image caption Didie Drogba ana haki ya kutabasamu,amerejesha kwenye jamii yake kile alichojaaliwa.

Mshambuliaji wa timu ya Chelsea F.C. Didier Drogba amezindua hospitali ya kwanza, kubwa na ya aina yake kati ya tano alizoahidi kuzijenga kama sehemu ya kujitolea kwa jamii yake .

Hospitali hiyo iko wilaya ya Attécoubé katika mji wa kibiashara wa Abidjan, hospitali hiyo imemgharimu nguli huyo wa kandanda kiasi cha dola milioni moja za kimarekani ili kukamilisha mjengo huo wa afya.

Hospitali hiyo ni maalumu kwa wanawake na watoto wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu .

Hospitali hiyo imejengwa katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba mia nane (800) huduma kadhaa zinapatikana ikiwamo chumba cha uchunguzi,

wodi ya wazazi,kitengo cha watoto,jengo la x-ray ,jengo la kisasa la maabara,duka kubwa la dawa,jengo la kulaza wagonjwa na jengo tengefu la wagonjwa.

Inakadiriwa hospitali hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa elfu hamsini kwa mwaka na hii ni kwa muujibu wa katibu mkuu wa wakfu wa Didier Drogba ,Guy Roland Tanoh ambaye ndiye msimamizi mkuu wa mradi huo.

Hospitali zingine nne zilizaahadiwa na mwanasoka huyo ziko katika hatua za ujenzi za mwisho mwisho kukamilika ambazo ziko nchini Ivory Coast

katika miji ya Yamoussoukro, San Pedro, Man na Korhogo na zinatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi ujao.

Image caption Drogba

Asasi hiyo ya Drogba foundation inaandaa chakula cha hisani mjini London mwezi huu wa April tarehe 18 ili kupata fedha za kukamilisha miradi hiyo.

Mshambuliaji huyo wa timu ya Chelsea na pia timu ya Elephants anabakia kuwa mchezaji na mfungaji bora na wa mfano wa kuigwa nchini mwake

pamoja na kwamba amestaafu kuichezea timu yake ya taifa,ambayo iliutwaa ubingwa wa kombe la mataifa ya AfriKa mwaka huu nchini Equatorial Guinea mnamo mwezi wa February.

Kazi nzuri Didier Drogba! .