Simba na Azam kupepetana ligi kuu

Image caption Kikosi cha watoto wa Msimbazi, Simba sports club

Baada ya Yanga kuchanja mbuga kuelekea ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara, sasa ni wazi vita ipo kati ya Simba na mabingwa watetezi, Azam FC ya kugombania nafasi ya pili.

Azam imekumbwa na droo tatu mfululizo na kubaki nafasi ya pili ikiwa na pointi 39, ikifuatiwa na Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi 35.

Kuelekea mechi za wikiendi, kocha wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic ameitangazia Azam vita ya kugombania nafasi ya pili ili kupata nafasi ya kuiwakilishi nchi katika michuano ya vilabu ya kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kuelekea katika vita hiyo, Azam na Simba zitakuwa katika viwanja tofauti wikiendi hii kutafuta pointi tatu muhimu.

Lakini kabla ya mechi zao, ligi hiyo inatarajiwa kuendelea Ijumaa kwa mchezo mmoja, wenyeji timu ya Stand United watawakaribisha maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Siku ya Jumamosi, Polisi Morogoro watawakaribisha Ndanda FC kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Jijini Mbeya wenyeji timu ya Mbeya City watawakaribisha timu ya Simba SC kwenye uwanja wa Sokoine , huku Azam FC wakiwakaribisha wakata miwa wa Kagera Sugar kwenye uwanja wa Chamanzi Complex.

Siku ya Jumapili, maafande wa timu ya Ruvu Shooting watawakaribisha maafande wenzao wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Mabatini - Mlandizi, huku jijini Mbeya wenyeji timu ya Prisons FC wakiwakaribisha wakata miwa wa Mtibwa Sugar.